Mapishi ni kitu ambacho nakipenda sana na huwa nakifanya kwa upendo sana. Naamini hata wewe unayesoma utakuwa ni mpenzi wa mapishi. Sasa wakati mwingine unaweza tamani upate kuku wa kuchoma na kuna namna nyingi sana za uchomaji wa kuku. Leo nakushirikisha namna ya kuchoma kuku mzima katika oven au katika jiko la kufunika.
Labda niseme hivi kuku huyu hachomwi na moto wa moja kwa moja ( direct heat) bali anaiva kwa joto tu. Na huwa inachukua hadi masaa 4-6 kuiva vizuri kwa vile huwa ni kuku mkubwa wa kilo mbili hadi mbili na nusu.
Kujua kama kuku ameiva vizuri huwa kuna vipima joto maalumu na huwa kama ukipima basi kwa ndani anatakiwa kufikisha nyuzi joto 180 F ; hapo anakuwa ameiva na nyama iko laini na sio kavu kabisa ( Juicy and tender).
Lakini sasa kama hauna kipima joto ni vema kuichoma kwa masaa 4 – 6 kwa hisia na kimapishi na macho – Kama unajua ni unajua tu. Maana hata mie mara nyingi hutumia hisia na macho kujua kama imeiva au lah.
MAHITAJI
- Kuku wa Kilo 2 mmoja
- Masala ya kuku choma ( waweza kutumia mahanjumati masala)
- Karoti 2 – Kata mapande makubwaa
- Limao 1
- Spinach – fungu mboja Chambua na safisha kata mapande makubwa
- Punje 5 za kitunguu swaumu – menya tu
- Jani moja kavu au bichi la rosemary
- Mafuta ya Kula vijiko 5
- Chumvi kwa kiasi upendacho
JINSI KUANDAA KUKU NA KUMCHOMA
- Kwanza ni kumuweka masala ( marination) – Katika masala uliyonayo ongeza mafuta ya kula, maji ya limao na chumvi. Kisha mpakae kuku mzima nje na ndani.
- Ile sehemu ya ndani ndio unaweka karoti , maganda ya limao baada ya kukamua juisi yake, spinach, rosemary, vitunguu swaumu. Ukisha vijaza ndani unaweza kufunga ile sehemu ya nyuma kwa kuishona na vijiti ya tooth picks. Vile vipapatio vikunje vilalie chini.
- Mfunike pembeni wakati viugo vinamwingia kuku vizuri andaa jiko lako kama ni oven basi ipate moto kufikia joto la juu likipasha joto juu na chini, kama ni mkaa hakikisha mkaa umewaka vema na kutengeneza joto.
- Tengeneza mfano wa kisahani kwa kutumia foil paper au tumia zile serving dish za aluminum. Muweka kuku akilalia mgongo kisha nyunyiza mafuta juu yake na umuweka katika jiko lako.
- Baada ya kumuweka ni kazi kwako kumuangalia kila baada ya nusu saa au saa lizima ukiongeza au kupunguza joto hadi atakapokuwa ameiva kabisa
No comments:
Post a Comment