Thursday, 7 June 2018

Samaki wa kupaka

 
 
 

Mahitaji

  • Samaki 2
  • Nazi 1
  • Vitunguu maji 1
  • Karoti 2
  • Vitunguu swaumu 1
  • Hiliki 1
  • Pilipili mbichi 1 (kama ni mpenzi wa pilipili, siyo lazima)
  • Nyanya 3
  • Ndimu 1
  • Chumvi Kijiko 1 kikubwa
  • Bizari
  • Foil paper
  • Vibanio vya kuchomea samaki

Maelekezo

Mie napendelea kula samaki mzima mzima bila kumkata. Huwa nahisi raha sababu naweza kumtafuna mwenyewe bila ya kuwa na kiambato kingine zaidi. Katika mapishi haya, utaelewa umuhimu wa kumla samaki mzima, maana hakuna utakachobakisha. Angalia tu usije kukwamwa na miba, maana utamu ukizidi unaweza kushangaa umemeza hadi miba ya samaki.
  • Andaa viungo vyako vyote, kisha saga nyanya, vitunguu maji, karoti, hiliki,vitunguu swaumu kwa pamoja.
  • Kuna nazi yako na uchuje tui zito.
  • Osha samaki kisha mchovye kwenye viungo.  Nyunyizia pilipili juu yake (hii si lazima kwa wale wasiokula pilipili). Ongeza chumvi na umkamulie ndimu.  Kisha acha samaki wako wakae kwa dakika kama 10 ili viungo vipate kuingia.
  • Rudia hivyo kwa idadi ya samaki ulionao.
  • Funga samaki kwenye foil. Banika au choma Samaki wako kwenye jiko la mkaa ( kama BBQ) au oven. Unaweza kuchoma kwa njia yeyote lakini nashauri kutumia jiko la mkaa pamoja na waya wa kuchomea. Weka moto mdogo sana kisha mbanike ili aweze kuiva kwa joto kiasi. Unaweza kumgeuza geuza ili aweze kuiva vizuri pande zote.
  • Anza kupika tui la nazi kwa kubandika chungu au sufuria jikoni. Koroga tui huku ukiwa unaongeza viungo ulivyosaga hapo awali - nyanya, vitunguu maji, vitunguu swaumu, hiliki, na karoti. Kisha ongeza ndimu na chumvi. Angalia usizidishe chumvi maana samaki ana chumvi pia. Usiache kukoroga ili kufanya tui kuwa laini kwa matokeo mazuri zaidi. Koroga mchanganyiko wa tui hadi likauke na kuwa kitu kimoja na viungo vyake.
  • Kama umetumia jiko la mkaa - Samaki akishaiva, mtoe kwenye foil, kisha chukua kibanio cha kukaangia samaki muweke na uanze kumnyunyuzia rojo juu yake.  Mgeuze na kuongeza rojo ya tui juu yake. Changanya vizuri hadi rojo liingie vizuri. Fanya hivi kisha muweke samaki kwenye moto mdogo ili kuhakikisha kuwa samaki, viungo na rojo vinaungana vizuri. Ukimaliza tenga samaki kwenye sahani tofauti.
  • Kama umetumia oven - Samaki akishaiva, mtoe kwenye foil, Chukua chombo (mfano sahani) kisha nyunyuzia rojo juu yake. Muweke samaki juu ya hiyo rojo na uendelee kuongeza rojo ya tui juu ya samaki wako. Changanya vizuri hadi rojo liingie vizuri. Ukishamaliza unaweza kumuweka samaki kwenye moto modogo ili kuhakikisha kuwa samaki na rojo vinaungana vizuri. Ukimaliza tenga samaki kwenye sahani tofauti.
  • Rudia hii hatua hiyo kwa samaki wote waliobaki.
  • Ukimaliza mboga yako iko tayari kuliwa. Ni vizuri ikiliwa ikiwa bado ya moto kwa kuleta ladha nzuri.
Unaweza kula mboga hii na wali, ugali, maandazi, chapati, au ukachanganya na mboga za majani.
Jirambee na ladha ya maisha..! Enjoy samaki wa kupaka.

No comments:

Post a Comment

JIFUNZE KUTENGENEZA TAMBI KWA MTINDO WA KIMOROKO

JIFUNZE KUTENGENEZA TAMBI KWA MTINDO WA KIMOROKO TAMBI HIZI NI MAARUFU SANA NCHINI MOROKO, NI RAHISI KUANDAA NA NI TAMU SANA KWA...